MREMBO anayedatisha katika video za nyimbo mbalimbali za Kibongo na mcheza filamu anayekuja kwa kasi, Agnes Gerald ‘Masogange’ ameponea chupuchupu kufa kwenye ajali mbaya ya gari na sasa hatamaniki midomo,
Masogange ambaye hivi karibuni ameanza kujipenyeza kwenye filamu, alikutwa na ajali hiyo akiwa ndani ya taksi akitokea nyumbani kwake Sinza Makaburini kwenda Kwaremmy kwenye mgahawa wa chakula wa Fast Food kutafuta mlo wa jioni.
Msanii huyo alisema kuwa ni wakati gari hilo likiwa linatafuta maegesho nje ya mgahawa huo ghafla lilitokea gari lingine lililokuwa katika mwendo wa kasi na kuligonga gari alilokuwemo.
Alisema alipata mshtuko na msukumo mkubwa uliomfanya ajigonge midomo kwenye kioo na kupasuka.
Aliongeza kwamba, mbaya zaidi baada ya ajali hiyo watu walilizunguka taksi wakiwemo vibaka ambao walitumia mwanya wa ajali kumkwapulia simu yake ya mkononi na fedha alizokuwa nazo (hakutaja kiasi).
“Baada ya kupata mzinga mimi nilijigonga kwenye kioo cha mbele cha gari na kupasuka midomo. Baada ya hapo vibaka waliniibia simu na fedha, wakatimka,” alisema Masogange.
Hata hivyo, Masogange alisema wasamaria wema walimchukua na kumpeleka Kituo cha Afya cha Serikali Palestina, Sinza ambako alishonwa nyuzi tano.
Akasema kwa taabu: “kikubwa kwa sasa namshukuru Mungu kwa kuwa ilikuwa ajali mbaya ambayo ingeweza kukatisha maisha yangu.”
No comments:
Post a Comment