Rogers Abdallah ambaye ni majeruhi wa ajali hiyo, akiwa Hospitali ya Mkoa wa Pwani, Tumbi Alieleza kuwa Regia ndiye aliyekuwa akiendesha gari hilo.
“Ilikuwa saa 5:15 asubuhi. Tulikuwa tunatokea nyumbani Mbezi Makabe tunakwenda Ruvu shambani. Tulipofika Ruvu darajani, alitaka kulipita lori lakini alipoanza kulipita, tukakutana uso kwa uso na lori lingine.
“Ili kulikwepa lori, ikabidi apindishe kulia kwa kulitoa gari nje ya barabara, bahati mbaya tairi la kushoto lilipasuka, hivyo gari kupinduka mara saba,” alisema Rogers.
Marehemu Regia alikuwa mlemavu wa mguu wa kulia, ilikuwaje akaendesha gari? Rogers “Mara kwa mara mimi ndiye huwa namuendesha lakini leo (juzi) alisema anaendesha mwenyewe na akichoka ndiyo nitamuendesha.”
Rogers aliendelea kusema kuwa ndani ya gari hilo lenye namba za usajili T 296 BSM, walikuwa ni watu nane na waliopoteza maisha ni wawili.
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha), John Heche, alisema kuwa mbali na Regia, mwingine aliyefikwa na mauti ni mhudumu wake anayeitwa, Teresia Simon.
Wabunge wa Chadema, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe (Mbunge wa Hai), walikuwemo Hospitali ya Tumbi ambako mwili wa Regia ulihifadhiwa kwa muda kabla ya kuhamishiwa Muhimbili.
No comments:
Post a Comment